Nafasi Ya Matangazo

July 29, 2015

Wajumbe wa Kamati ya Media Car Wash for Cancer wakimkabidhi Adol Kivamwo mfano wa hundi wenye thamani ya shilingi Milioni 10 kwaajili ya kusaidia matibabu yake ya saratani. Makabidhiano hayo yalifanyika jijini Dar es Salaam hii leo.
************
Waandishi wa habari watatu, Adolf Simon Kivamwo, Athumani Hamisi na Danstan Bahai wamekabidhiwa jumla ya TZS 20m/- kwa ajili ya kulipia gharama za matibabu  yao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Harambee ya Kuwasaidia waandishi wanaougua maradhi mbali mbali, Bw. Benjamin Thompson alisema kuwa fedha hizo ni matunda ya harambee ya Media Car Wash for Cancer Campaign, inayoendelea nchini.

Kama tujuavyo, kwa kuanzia, wanahabari kutoka vyombo mbalimbali Jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na wadau wengine waliosha magari kwenye viwanja wa Leader Club Julai 4, 2015.

Alisema katika harambee hiyo jumla ya 31m/-, zilipatikana, ambapo kati ya fedha hizo, ndizo wagonjwa wamegawiwa.

“Malengo yetu ya awali yalikuwa kwamba tuwachangishe fedha kwa ajili ya wenzetu wagonjwa, pia kiasi kingine kitumike kuwaingiza baadhi ya wanahabari kwenye mifuko rasmi ya Bima ya Afya. Na ndivyo tulivyofanya leo hii,” alisema.

Bw Thompson alisema kiasi kilichosalia kitatumika kuwaingiza waandishi wa habari 100 katika mpango wa kulipia matibabu kupitia mfuko wa Bima ya Afya, yaani  NHIF.” Alisema.

Alisema lengo la harambee hiyo ni kukusanya jumla ya 100m/- kabla ya mwezi Disemba 2015 na kazi yake kubwa itakuwa kuwahudumia wanahabari wasiojiweza kwa sababu ya kusumbuliwa na maradhi mbalimbali.

Pia pesa zitokanazo na harambee hiyo zitasaidia kuanzisha mkakati wa mkubwa wa kuhakikisha wanahabari wote nchini wanaingizwa kwenye mfuko wa Bima ya Afya.

“Lengo letu ni kuhakikisha wanabari wana kinga za afya zao,ili tukomeshhe huu mtindo wa kuchangiana mara kwa mara kila mmoja anapougua,”alisema na kuongeza kuwa  watakaohusika katika zoezi hilo, ni wale wasioajiriwa pamoja na wasioajiriwa lakini hawana huduma ya Bima ya Afya.

Ili kuendeleza mchakakato wa kufikia lengo kuu, wanahabari Kanda ya Ziwa kwa kushirikiana na wenzao wa Jijini Dar es Salaam, Agost 15 mwaka huu, wataosha magari kwenye viwanja vya Furahisha Jijini Mwanza.

Tunaomba wadau mbalimbali waungane nasi kwenye hili,ikiwemo kulipia gharama mbalimbali ukiwemo usafiri kwenda na kurudi Mwanza,hoteli, matangazo ya radio na mabango.

Wakati huo huo Bw Thompson amesema kutakuwa mkutano wa wadau habari Jumamosi Agost 1, mwaka huu utakaofanyika Msimbazi Centre Jijini Dar es Salaam kwa jili ya kuanzisha mchakato wa usajili wa rasmi wa kampeni hii.

“Tunaomba wanahabari wote nchini watakaoweza kuhudhuria wasikose kufika, maana hapa ndipo juhudi za ukombozi wa kiafya kwa wanahabari zitakapoanzishwa rasmi,” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo alisema kuwa Kamati yake imewashirikisha wahariri wote nchini katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa na kwamba viongozi hao wa vyumba vya habari ndio waliotoa majina hayo kwa kamati.

Benjamin  Andongolile Thompson
Mwenyekiti Kamati ya Maandalizi
Posted by MROKI On Wednesday, July 29, 2015 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo