Nafasi Ya Matangazo

February 07, 2017



Shirika la ndege la kitanzania Precision Air limefanikiwa kufaulu kwa mara nyingine ukaguzi wa IOSA na kupata  cheti cha Usalama (IOSA) kitolewacho na shirikisho la kibiashara la mashirika ya ndege duniani (IATA). Precision Air imepata cheti hicho ikiwa ni kwa mara ya sita mfululizo (2006, 2008, 2010 na 2012, 2014 na 2016) 

Mafanikio haya yamepatikana baada ya kufanyiwa uhakiki wa usalama ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili. IOSA ni mkakati utambulikao na kukubalika  kimataifa kwa ukaguzi wa utawala na usimamizi wa shughuli za mashirika ya ndege katika maswala ya usalama.

Cheti hicho hutolewa kama ishara ya shirika kukaguliwa na kufuzu kuwa na viwango vinavyo kubalika kimataifa. Cheti cha sasa kitadumu kwa miaka miwili hadi Tarehe 22 Septemba 2018 ambapo Precision Air itafanyiwa ukaguzi tena. 

Akizungumzia mafanikio hayo Mkurugenzi mtendaji wa Precision Air Bi.Sauda Rajab, amesema Precision Air imejizatiti na kuhakikisha inatoa huduma za uhakika na salama kwa wateja wake na kwamba sikuzote usalama wa abiria na ndege  ni kipaumbele cha kwanza kwa shirika.

“Kupatikana kwa cheti hiki kwa mara nyingine kuna maana kubwa kwetu sisi kama shirika na sekta ya anga kwa ujumla, ni uthibitisho wa kiwango cha ubora wa huduma za usafri wa anga kinachotolewa na shirika la kitanzania.” Ameongeza Bi.Rajab

IATA ni shirikisho la kibiashara la kimataifa la mashirika ya ndege linalowakilisha mashirika zaidi ya 240 yanayosafirisha zaidi ya asilimia 84% ya wasafiri wa anga duniani. Shughuli za IATA zinasaidia uundwaji wa sera za mambo muhimu katika sekta ya anga pamoja na maendeleo ya sekta hiyo katika nyanja ya usalama.

Shirika la ndege la Precision Air ndilo shirika pekee la kitanzania lenye cheti cha IOSA na mwanachama pekee wa shirika hilo kwa sasa. Precision Air inafanya safari zake kutokea Dar es Salaam ambapo ndipo makao makuu yake kwenda Mwanza,Arusha,Kilimanjaro,Bukoba, Musoma, Kigoma,Tabora,Mtwara, Zanzibar na Nairobi.
Posted by MROKI On Tuesday, February 07, 2017 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo