Nafasi Ya Matangazo

August 29, 2016

Bw: Israel Chasosa- Mkurugenzi Mtendaji
Benki ya Akiba imetangaza gawio la shilingi 75 kwa hisa kwa wanahisa wake kwa mwaka unaoishia Desemba 31, 2015.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Akiba, Israel Chasosa alisema hili no ongezeko la zaidi ya asilimia 100 ikilinganishwa na gawio la shilingi 30 kwa hisa lililotolewa mwaka 2014.

Chasosa alisema kutolewa kwa gawio hilo ni matokeo ya benki hiyo kufanya vizuri kibiashara ikiwemo kupata faid tangia kuanzishwa kwake miaka 18 iliyopita.

 “Wakati wa kuamua ulipaji wa gawio, bodi ya benki yetu huangalia zaidi uwiano kati ya gawio hilo na kubakiza faida nyingine ili iweze kurudishwa kwenye uendeshaji wa benki kwa ajili ya kukuza biashara,” alisema.

Chasosa alibainisha kwamba hii ni mara ya tatu mfululizo kwa benki hiyo kutoa gawio kwa wanahisa wake.

“Hii ni ishara kwamba wanahisa wetu wana imani kubwa na benki yetu kwani tumekuwa tukipata faida endelevu kwa muda wote ambao tumekuwa kwenye biashara,” alisema.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2015 iliyokaguliwa, benki hiyo ilipata faida ghafi ya shilingi bilioni 5.3 mwaka jana, ambapo kiwango kama hicho kilipatikana katika kipindi cha mwaka 2014.

Ripoti hiyo inaonyesha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2015 benki hiyo ilitoa mikopo ya shilingi bilioni 107.3 ikilinganishwa na shilingi bilioni 77.2 zilizokopeshwa mwaka 2014.

Rasilimali za benki ziliongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 163.7 mwaka 2015 ikilinganishwa na shilingi bilioni 135.3 kwa mwaka 2014 wakati mtaji wa benki ulikuwa na kufikia bilioni 19.3 mwaka jana kutoka bilioni 16 mwaka 2014.

Pato kwa kila hisa lilikuwa ni shilingi 466 mwaka jana ikilinganishwa na shilingi 400 mwaka 2014.

Chasosa alisema mwaka 2015 ulikuwa mwaka wa mageuzi makubwa kwa benki hiyo kwani kulikuwepo na ubunifu mkubwa ambao ulisababisha bidhaa na huduma zake kuongezeka.

“Akiba inaendeshwa katika mazingira ya ushindani mkubwa kwani hadi sasa kuna benki zaidi ya 50 na taasisi za fedha. Benki yetu imeendelea kuhakikisha kwamba huduma zake zinawafikia walengwa ambao ni wale wenye vipato vya chini na kati hasa wale ambao hawajafikiwa na huduma za benki,” alisema.

Amesema mwaka huu, benki imejidhatiti kuhakikisha kwamba inapanua huduma zake kupitia wakala wa benki (agency banking) ili kuhakikisha kwamba walengwa wote wanafikiwa.

Pia matumizi ya huduma za benki kwenye simu za mikononi (Akiba Mobile) imeboreshwa zaidi ili kuwafanya wateja wa benki hiyo kupunguza gharama na muda, kupata huduma kwani ni rahisi kutumia.
Posted by MROKI On Monday, August 29, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo