Nafasi Ya Matangazo

February 08, 2016

Gari STK 9442 alilokua akisafiria kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam mke wa Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, Mama Tunu Pinda likiwa limeharibika vibaya baada ya kupata ajali hii leo jioni eneo la Mkundi mkoani Morogoro. 
MKE wa Waziri Mkuu mstaafu, Tunu Pinda  na wenzake watatu akiwemo dereva wa gari wamenusurika kifo baada ya gari alilokuwa akisafiria kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam kupinduka kutokana na kumgonga mwendesha bodaboda eneo la Mkundi Manispaa ya Morogoro katika barabara kuu ya Dodoma – Morogoro.

Ajali hiyo ilitokea saa nane mchana leo katika eneo hilo wakati gari lenye namba za usajili STK 9442 aina ya Toyota Land Cruiser lilipomgonga mwendesha bodaboda akiwa na pikipiki yenye namba MC 647 BBA na kupinduka.

Mke huyo wa Waziri Mkuu mstaafu na wenzake watatu walijeruhiwa na walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kupatiwa matibabu na kuchunguzwa afya zao.  Mama Pinda na wenzake waliruhusiwa kuendelea na safari.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk Rita Lyamuya alithibitisha kuwapokea majeruhi hao akiwemo Mama Tunu Pinda ambaye hakuumia sana licha ya kupata maumivu kifuani.

Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, mbali na Mama Tunu, majeruhi wengine ni dereva Angelo Mwisa (50), Gilbert Sampa (40) pamoja na mlinzi wa mke huyo wa Pinda, Gaudencia Tembo.

Alisema walipata majeraha madogo madogo kwenye mbavu na kifuani na baaada ya kupata matibabu wameruhusiwa kuendelea na safari ya kwenda Dar es Salaam. “Tumepokea majeruhi wanne akiwemo Mama Pinda hawakuumia sana, ni majeraha madogo ambapo dereva ameumia kidogo usoni na hali zao sio mbaya.

Jioni hii wanaendelea na safari, mikanda waliokuwa wamejifunga imesaidia kutopata majeraha makubwa,” alisema Dk Lyamuya. Alisema hospitali hiyo pia ilipokea mwili wa dereva wa bodaboda ambaye aligongwa katika eneo la tukio hilo na jina lake hadi jana lilikuwa halijatambuliwa.


Ajali hiyo ilitokana na mwendesha bodaboda aliyekatisha barabara kuu kutoka upande mmoja wa barabara kwenda mwingine bila kuchukua tahadhari na hivyo kusababisha kugongwa na gari hilo na kupinduka.
Posted by MROKI On Monday, February 08, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo