Nafasi Ya Matangazo

November 25, 2015

Na Father Kidevu Blog
Rais John Magufuli amesitisha  maadhimisho ya siku ya Ukimwi kitaifa ambayo yalikuwa yafunguliwe mkoani Singida leo na kufikia kilele chake Desemba mosi mwaka huu mjini humo.



Badala yake Rais Dk Magufuli ameagiza fedha zote ambazo zilitengwa na serikali pamoja na wahisani mbalimbali kwaajili ya maadhimisho hayo zielekezwe kununua dawa kwaajili ya waathirika wa Ukimwi na  vitendanishi.



Akizungumza na moja kwa moja na Televisheni ya Taifa (TBC), Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Dk Fatma Mrisho, alisema serikali imeagiza jana wakati tayari mkuu wa Mkoa wa Singida akiwa ameshafungua maonesho ya maadhimisho hayo.



“Serikali imesitisha maadhimisho ya mwaka huu Singida na badalayake fedha zilizopangwa kwaajili ya maadhimisho ziende zikanunue dawa za virusi vya Ukimwi, dawa za kudhibiti maambukizi ya ukimwi na vitenganishi,” alisema Mrisho.




Dk Mrisho alisema kuwa tayari taarifa za kusitisha maadhimisho hayo zimesha wafikia washiriki na wale walio kuwa njia kuelekea Singida wamegeuza.  SOMA ZAIDI BOFYA HAPA.
Katika maadhimisho ya mwaka huu serikali ilitenga kiasi cha shilingi  Milioni 18 kwaajili ya maadhimisho hayo huku kila mshiriki katika maonesho hayo akiachangia kiasi cha sh laki tano.



Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Dk Fatma Mrisho alisema maadhimisho ya mwaka huu yakuwa yatanguliwe na maonesho ya wadau yatakayojumuisha huduma mbalimbali zikiwamo za utoaji elimu na burudani.



Dk Mrisho alisema huduma nyingine zilizopangwa kutolewa katika maadhimisho hayo ya wiki moja ni upimaji wa hiari wa watu zaidi ya 3,500  wanaoishi na virusi vya Ukimwi na utoaji ushauri nasaha, upimaji wa shingo ya uzazi, sukari, uzito, damu na kupata elimu itakayotolewa kupitia vikundi vya sanaa na burudani.



Maadhimisho ya mwaka huu yanachagizwa na kaulimbiu ya ‘Tanzania bila maambukizi mapya ya VVU, vifo vitokanavyo na Ukimwi na ubaguzi na unyanyapaa inazewekana.’



Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake hivi karibuni kuwa maadhimisho hayo yanatarajiwa kuanza Novemba 24 mwaka huu kwenye viwanja vya Peoples Club ambapo uzinduzi utakuwa Novemba 25 kabla ya kilele, Desemba mosi.



Hii ni mara ya tatu tangu Rais Dk Magufuli aingie madarakani kuzuia maadhimisho yanayogharimu fedha nyingi na sherehe na fedha zake kuelekeza ikanunulie vifaa tiba mahospitalini.



Awali Rais aliagiza fedha zilizotengwa kwaajili ya hafla ya uzinduzi wa Bunge zaidi ya shilingi Milioni 225 ziende kununulia vitanda vya hospitali ya taifa Muhimbili.



Aidha Rais pia alisitisha maadhimisho ya siku ya Uhuru Desemba tisa mwaka huu na badala yake watu wafanye kazi katika maeneo yao ya kazi hasa usafi wa mazingira.
Posted by MROKI On Wednesday, November 25, 2015 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo