Nafasi Ya Matangazo

October 27, 2014



Mkuu wa Wilaya ya Arusha John Mongela akiongea jambo wakati akifungua rasmi mafunzo  ya siku mbili kuhusu masuala ya jotoardhi  kwa washirki kutoka nchi zilizo katika bonde la Ufa . Mafunzo hayo yanatangulia kabla ya ufunguzi rasmi wa Kongamano la Tano la Kimataifa la Jotoardhi litakalofunguliwa tarehe 29 Oktoba, 2014 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal.



Baadhi ya washiriki wanaohudhuria mafunzo kuhusu masuala la jotoardhi wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Arusha John Mongela hayupo pichani wakati akifungua rasmi mafunzo hayo.



Na Asteria Muhozya, Arusha
Imeelezwa kuwa, nguvu ya nishati mchanganyiko ikiwemo jotoardhi ni kichocheo na kipimo cha maendeleo kwa nchi yoyote kutokana na umuhimu wa nishati hiyo kwa  shughuli mbalimbali  zikiwemo za uchumi na  viwanda.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa  Wilaya ya Arusha John Mongela wakati akifungua mafunzo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo, kuhusu masuala yanayohusu  jotoardhi yaliyoanza leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).

Mafunzo hayo yanashirikisha washiriki takriban 150 kutoka nchi mbalimbali za Afrika zilizo katika bonde la ufa na  nchi nyingine duniani.

Aidha, ameongeza kuwa, mafunzo hayo ni muafaka kwa Tanzania kutokana na uzoefu ambao washiriki wataupata kutoka nchi nyingine ambazo zimepiga hatua katika masuala ya jotoardhi kama Kenya na Ethiopia  ambazo zimechangia katika gridi ya Taifa ya nchi zao kiasi cha megawati 500 za nishati ya umeme unaotokana na jotoardhi.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia nishati jadidifu, Wizara ya Nishati na Edward Ishengoma, ameeleza kuwa, mafunzo hayo na uwepo wa kongamano hilo kwa Tanzania kuna manufaa makubwa.

Ishengoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la tano la Kimataifa la Jotoardhi alitaja manufaa hayo kama kutangaza hazina kubwa ya jotoardhii iliyopo Tanzania, jambo ambalo litasaidia kuvutia wawekezaji na taasisi zinazofanya utafiti wa masuala ya jotoardhi.

Ameongeza kuwa, nishati ya jotoardhi ni nishati isiyokwisha hivyo uwepo na matumizi yake yatasaidia katika ukuaji wa viwanda ikiwemo kuchangia katika sekta za kilimo na manufaa yake ni makubwa  kimaendeleo.

“Jotoardhi ni chazo ambacho hakiishi. Uzalishaji wake hauna mwisho na una manufaa makubwa. Tanzania tunataka kukiendeleza chanzo hiki kama wenzetu Kenya na Ethiopia”amesisitiza Ishangoma.


Aidha, mafunzo hayo ni mwendelezo wa shughuli mbalimbali zitakazofanyika katika kongamano la tano la Kimataifa la Jotoardhi litakalofunguliwa rasmi tarehe 29 Oktoba, 2014, na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal.

Washiriki wa kongamano hilo pia watapata fursa ya kutembelea katika maeneo yenye dalili za jotoardhi ikiwemo Ngorongoro na Manyara lakini pia watapata nafasi ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini.
Posted by MROKI On Monday, October 27, 2014 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo