Nafasi Ya Matangazo

August 19, 2014

MABASI mawili yamegongana uso kwa uso wilayani Sikonge mkoani Tabora na kuua abiria 13, wakiwemo madereva wa mabasi hayo na kujeruhi wengine 73. 

Moja ya mabasi hayo, lilikuwa likitokea mkoani Mwanza kwenda Mpanda na lingine likitokea mkoani Mbeya kwenda Mwanza. Taarifa kutoka eneo la tukio, ilieleza kuwa mabasi hayo yalipata ajali hiyo leo saa 10.05 jioni katika eneo la Mlogoro, kilometa tatu kabla ya kuingia katika mji wa Sikonge. 

 Mabasi hayo moja linamilikiwa na Kampuni ya AM Investment Namba T 803 ATN, lililokuwa likitokea Mwanza kwenda Mpanda. Lingine ni mali ya kampuni ya Sabena Namba T 110 ARV, lililokuwa likitokea Mbeya kwenda jijini Mwanza. Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana jioni, Kaimu Mganga wa Wilaya ya Sikonge, Dk John Buswelu, alisema hospitali hiyo ilikuwa imeshapokea miili 13 ya abiria waliokufa, huku mmoja ukiwa kiwiliwili bila kichwa. 

 Shuhuda wa ajali hiyo aliyekuwa sehemu ya tukio, Suleimani Kambuzi alidai majeruhi waliotolewa katika ajali hiyo, walikuwa zaidi ya 70. Alidai wengine walikuwa wakiendelea kutolewa na kupelekwa hospitalini. Gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda, ambaye alikiri kufahamu kutokea kwa ajali hiyo. Aliongeza kuwa taarifa rasmi ataitoa leo.

 Ajali hiyo imetokea wakati Watanzania hawajasahau ajali iliyotokea wakati wa Sikukuu ya Idd el Fitri mwezi uliopita, na kuua watu 17 katika eneo la Pandambili wilayani Kongwa mkoani Dodoma. Ajali hiyo ilihusisha basi la kampuni ya Moro Best, lenye namba za usajili T 258 AHV lililokuwa likitoka Mpwapwa kwenda Dar es Salaam. Basi hilo liligongana uso kwa uso na lori la mizigo, lenye namba za usajili T820 CKU -T 390 CKT, lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Posted by MROKI On Tuesday, August 19, 2014 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo